18 Aprili 2025 - 20:57
Source: Parstoday
Trump kufunga balozi 30 za Marekani duniani, zaidi ya nusu ziko Afrika

Utawala wa Trump unapanga kupunguza makumi ya balozi za Marekani duniani kote, ambapo umependekeza kufunga balozi na balozi ndogo karibu 30, zaidi ya nusu zikiwa barani Afrika.

Mpango huo ni sehemu ya mpango mpana wa serikali ya Trump wa kupunguza bajeti ya Wizara ya Mshauri ya Kigeni ya Marekani kwa karibu asilimia 50 ikilenga kupunguza misaada  ya Washington kwa nchi mbalimbali duniani kwa takriban asilimia 75.

Waraka kutoka Wizara ya Mshauri ya Kigeni ya Marekani umeeleza kuwa, balozi zilizopendekezwa kufungwa ni  pamoja na balozi za Marekani nchini Lesotho, Eritrea, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Kongo, Gambia na Sudan Kusini. Zaidi ya hayo, balozi ndogo za Marekani huko Durban, Afrika Kusini, na Douala nchini Cameroon zinatazamiwa kufungwa, huku majukumu yao yakitazamiwa kuhamishiwa katika nchi jirani.

Wakosoaji wa pendekezo hilo la serikali ya Trump wameelezea wasiwasi wao kwamba kupunguza uwepo wa Marekani kidiplomasia  barani Afrika kunaweza kupunguza ushawishi wa nchi hiyo katika bara hilo, hasa wakati huu ambapo mataifa mengine yenye nguvu duniani, kama vile Uchina, yanaendelea kupanua uwepo wao barani Afrika.

Wanasema kuwa, kufungwa balozi na balozi ndogo za Marekani katika nchi za Kiafrika kunaweza kuzuia uhusiano wa kidiplomasia na ushirikiano wa kiuchumi n.k.

Mpango huu wa serikali ya Rais Donald Trump pia unajumuisha uwezekano wa kufungwa balozi barani Ulaya kama kufungwa balozi za Washington huko Malta na Lusembourg na pia balozi zake ndogo katika miji mbalimbali ya Ulaya na Asia. 

Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani imesema kuwa mabadiliko haya ni sehemu ya juhudi kubwa zaidi za kurahisisha shughuli za serikali na kubana matumizi.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha